slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Wednesday, May 23, 2018

WAZIRI KIGWANGALLA AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA ITALIA NCHINI, ROBERTO MENGONI

 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Balozi wa Italia nchini, Roberto Mengoni ofisini kwake Jijini Dodoma leo ambapo wamekubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye tafiti za binadamu wa kale katika eneo la Olduvai, kuboresha utoaji wa elimu hususan ya mapishi ya vyakula vya Kiitaliano katika Chuo cha Taifa cha Utalii na Utangazaji wa vivutio vya utalii nchini. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akiwa kwenye picha ya pamoja na Balozi wa Italia nchini, Roberto Mengoni baada ya mazungumzo ofisini kwake Jijini Dodoma leo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla akiagana na Balozi wa Italia nchini, Roberto Mengoni baada ya mazungumzo ofisini kwake Jijini Dodoma leo.

MAPORI MATANO YA AKIBA MKOANI KAGERA NA GEITA KUPANDISHWA HADHI YA KUWA HIFADHI ZA TAIFA (NATIONAL PARKS)

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Hamisi Kigwangalla akizungumza bungeni alipokuwa akijibu hoja wa wabunge waliochangia mjadala wa bajeti wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma juzi.

............................................................

Wizara ya Maliasili na Utalii imetangaza kuanza mchakato wa kuyapandisha hadhi Mapori ya Akiba ya Burigi, Kimisi, Biharamulo, Ibanda na Rumanyika kuwa Hifadhi za Taifa.

Mchakato huo tayari umeungwa mkono na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Hayo yameelezwa juzi bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla wakati akihitimisha mjadala wa bajeti wa makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019.

“Mheshimiwa Spika, ninaomba kulitaarifu Bunge lako tukufu kuwa  Mhe. Rais ameridhia ombi letu la kupandisha hadhi Mapori ya Akiba ya Burigi, Kimisi, Biharamulo, Ibanda na Chief Rumanyika kuwa Hifadhi za Taifa, kipekee namshukuru sana Mhe. Rais kwa kuridhia ombi letu hilo” amesema Dkt. Kigwangalla.

Amesema kufuatia hatua hiyo, wizara yake inaanzisha mchakato rasmi wa kukamilisha taratibu  za kupandisha hadhi mapori hayo ili kupanua wigo wa vivutio vya utalii katika kanda ya Kaskazini Magharibi na hivyo kufikia azma ya Serikali kuongeza idadi ya watalii kufikia milioni 8 na mapato ya dola za kimarekani bilioni 16 katika kipindi cha miaka 7 ijayo.

Inaelezwa kuwa mchakato huo utapitia hatua mbalimbali ikiwemo kuwashirikisha wadau husika kupata maoni yao, mapendekezo kuwasilishwa baraza la mawaziri kabla ya kujadiliwa bungeni na hatimaye kuwasilishwa kwa Mhe. Rais kwa ajili ya kuidhinishwa kuwa Sheria kamili ya kupandisha hadhi mapori hayo.

Akizungumzia mikakati mingine mipya ya kuboresha sekta ya maliasili na utalii itakayotekelezwa, Dkt. Kigwangalla amesema ni pamoja na kuanzisha mamlaka ya usimamizi na uendelezaji wa utalii wa fukwe nchini, kuhuisha maeneo ya vivutio vya Mambo ya Kale na kuviunganisha katika 'package' moja ya utalii na vivutio vya wanyamapori.

Mikakati mingine ni kuunda mfumo mmoja funganishi wa TEHAMA uitwao "MNRT Portal" kwa ajili ya kutoa leseni na vibali, ukusanyaji wa takwimu na mapato kutoka vyanzo mbalimbali vya sekta ya maliasili na utalii, ambapo utaunganishwa na mifumo mingine ya Serikali iliwemo GePG, NIDA, TIRA, BRELA, TRA na NBS.

Amesema mikakati mingine ni kuanzisha Jeshi Usu, Utambulisho wa Utalii wa Tanzania Kimataifa ujulikanao kama "Tanzania, Unforgettable", kufungua utalii wa kanda ya kusini, kuanzisha mwezi wa maadhimisho ya Urithi wa Mtanzania "Urithi Festival"  (Septemba), kuhuisha sheria za TANAPA, TAWA na TFS, pamoja na kuunda kanuni mpya za kusimamia vizuri sekta hizo.

Pori la Akiba Burigi lina ukubwa wa kilomita za mraba 2,941 katika wilaya za Karagwe, Muleba na Ngara mkoani Kagera, wakati Pori la Kimisi likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 1,030 katika wilaya za Ngara na Karagwe mkoani humo.

Pori la Akiba Biharamulo lina ukubwa wa kilomita za mraba 731 katika wilaya ya Muleba mkoani Kagera na wilaya ya Chato mkoani Geita, huku Pori la Akiba Ibanda likiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 200 na Pori la Akiba Rumanyika kilomita za mraba 800 katika wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera.

Mapori haya yapo katika ukanda muhimu wa kuunganisha watalii kutoka ikolojia za Magharibi na Mashariki ambapo uwanja wa ndege wa Chato utakuwa muhimu katika kutoa mawasiliano.

Mapori hayo ambayo yanasimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA sasa yatakuwa chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania - TANAPA punde baada ya mchakato wa kuyapandisha hadhi kukamilika. 

Bunge limeidhinisha Sh. bilioni 115.794 kwa ajili ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2018/2019 ambapo Sh. bilioni 85.816 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Sh. bilioni 29,978 ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo. 
  Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza bungeni alipokuwa akijibu hoja wa wabunge waliochangia mjadala wa bajeti wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma juzi.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Hamisi Kigwangalla na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga wakipongezwa na wabunge mbalimbali baada ya bajeti ya wizara yao kupitishwa na Bunge juzi jioni.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Maj. Gen. Gaudence Milanzi (kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa - TANAPA na Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali George Waitara (katikati) na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania - TAWA, Meja  Jenerali (Mstaafu) Hamis Rajabu SEMFUKO wakiwa kwenye picha ya pamoja nje ya ukumbi wa Bunge muda mfupi baada ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitishwa na Bunge.
 Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt Hamisi Kigwangalla, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, Katibu Mkuu, Maj. Gen. Gaudence Milanzi, Naibu Katibu Mkuu, Dkt. Aloyce Nzuki, Wakuu wa Idara, Vitengo na Taasisi pamoja na wafanyakazi wa wizara hiyo baada ya bajeti ya wizara yao kupitishwa na Bunge juzi jioni. 

Sunday, May 13, 2018

MADHIMISHO YA KIMONDO CHA MBOZI KUFANYIKA KWA MARA YA KWANZA MWEZI JUNI, 2018

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akiangalia Kimondo cha Mbozi alipotembelea kijiji cha Ndolezi, wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana kwa ajili ya kuangalia maandalizi ya maadhimisho ya siku ya kimondo duniani yatakayofanyika Juni 28 hadi 30 mwaka huu. Kimondo cha Mbozi ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika na kinakadiriwa kuwa na tani 12 na mchanganyiko wa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11.

Na Hamza Temba-WMU-Songwe
..........................................................................
Mkoa wa Songwe kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wengine wa uhifadhi na maendeleo utafanya maadhimisho ya siku ya Kimondo cha Mbozi kwa mara ya kwanza katika historia kwenye Kijiji cha Ndolezi Kata ya Mlangali, wilayani Mbozi kuanzia Juni 28 hadi 30 mwaka huu .

Maadhimisho hayo yataenda sambamba na maadhimisho ya siku ya Vimondo duniani ambayo yaliazimiwa kufanyika Juni 30 kila mwaka na kikao cha Umoja wa Mataifa cha tarehe 6 Desemba, 2016.

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho pia kiliazimia tarehe hiyo kuwa siku ya kuelimisha umma kuhusu elimu ya anga na mafanikio ya tafiti mbalimbali yaliyopatikana kuhusu elimu hiyo, kutambua juhudi zilizofanyika, kuweka sheria za kimataifa na kutoa tahadhari juu ya athari zinazoweza kutokea endapo dunia itafanya uharibifu juu ya anga.

Taarifa hiyo imetolewa jana katika Kijiji cha Ndolezi wilayani Mbozi na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Herman Tesha wakati akiwasilisha taarifa ya maandalizi ya maadhimisho hayo kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga ambaye alitembelea kituo hicho kwa ajili ya kukagua shughuli za maandalizi.

Amesema lengo la maadhimisho hayo ni kutangaza Kimondo kama kivutio muhimu cha utalii mkoani Songwe pamoja na vivutio vingine vya mkoa huo kwa ujumla ili kutoa fursa ya uwekezaji kwenye sekta ya utalii mkoani humo. 

Amesema maadhimisho hayo yataenda sambamba na kongamano la uwekezaji na sayansi ya vimondo, maonesho ya malikale, maonesho ya kiutamaduni, mashindano ya riadha (Kimondo Marathon), mashindano ya netiboli na mpira wa miguu (Kimondo Ligi).

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema Serikali kupitia Wizara yake itashiriki kikamilifu katika maadhimisho hayo kwa kushirikiana na mkoa wa Songwe na wadau wengine ili kuhakikisha kivutio hicho cha Kimondo kinajulikana zaidi ndani na nje ya nchi na hatimaye kiongeze idadi ya watalii na mapato.

Amesema wizara yake ina mkakati maalum wa kuimarisha kituo hicho cha utalii ambapo hivi sasa imeshajenga kituo maalum cha taarifa ambacho kimegharimu zaidi ya Shilingi milioni 400 za Kitanzania. 

Aidha, amesema kupitia mkakati mpya wa wizara wa kuimarisha na kuvijengea uwezo vituo vya malikale nchini kwa kuzishirikisha taasisi za uhifadhi wa wanyamapori na misitu, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanapa litashirikiana na kituo hicho kwa kuimarisha miundombinu pamoja na utangazaji. 

Nao wananchi wa kijiji cha Ndolezi wakizungumza kwa nyakati tofauti hawakusita kuonyesha furaha zao kuhusu maendeleo ya eneo hilo na kuahidi kutoa ushirikiano kwa Serikali katika mipango na miradi mbalimbali itakayoanzishwa katika eneo hilo kwa faida ya pande zote mbili.

Katika hatua nyingine, baada ya kuhitimishwa kwa ratiba za Mwenge wa Uhuru wilayani Mbozi, wakimbiza Mwenge Kitaifa walilazimika kutumia fursa ya uwepo wao wilayani humo kwenda kutalii kwenye kivutio cha Kimondo wakati wa usiku wakiongozwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga. 

Kimondo cha Mbozi kilianguka mwaka 1840 kutoka kwenye obiti yake huko angani huku kikikadiriwa kuwa na tani 12 na mchanganyiko wa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11. Kimomdo hicho ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika na cha nane duniani kati ya vimondo 600 vilivyodondoka maeneo mbalimbali ulimwenguni, sifa yake kubwa ni kuwa na ubaridi wakati wote hata mchana wa jua kali.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akikagua mpaka wa eneo la kituo cha kimondo na vijiji jirani alipotembelea kituo hicho cha utalii  katika kijiji cha Ndolezi, wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana kwa ajili ya kuangalia maandalizi ya maadhimisho ya siku ya kimondo duniani yatakayofanyika Juni 28 hadi 30 mwaka huu. Kimondo cha Mbozi ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika na kinakadiriwa kuwa na tani 12 na mchanganyiko wa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akikagua kituo cha taarifa cha Kimondo cha Mbozi alipotembelea kituo hicho cha utalii  katika kijiji cha Ndolezi, wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana kwa ajili ya kuangalia maandalizi ya maadhimisho ya siku ya kimondo duniani yatakayofanyika Juni 28 hadi 30 mwaka huu. Kimondo cha Mbozi ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika na kinakadiriwa kuwa na tani 12 na mchanganyiko wa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza na baadhi ya watalii wa ndani waliotembelea kituo cha utalii cha kimondo katika kijiji cha Ndolezi, wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana. Nyuma yao ni jengo jipya la kituo cha taarifa ambalo ujenzi wake umekamilika.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watalii wa ndani waliotembelea kituo cha utalii cha kimondo katika kijiji cha Ndolezi, wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana. Nyuma yao ni jengo jipya la kituo cha taarifa ambalo ujenzi wake umekamilika. Kimondo cha Mbozi ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika na kinakadiriwa kuwa na tani 12 na mchanganyiko wa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (nyuma kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wakimbiza Mwenge kitaifa, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Ernest Palingo (kushoto) na waratibu wa Mwenge mkoa wa Songwe mbele ya Kimondo cha Mbozi katika kijiji cha Ndolezi, wilaya ya Mbozi mkoani Songwe jana usiku baada ya shughuli za Mwenge. Kimondo hicho ni cha pili kwa ukubwa barani Afrika na kinakadiriwa kuwa na tani 12 na mchanganyiko wa madini ya Chuma 90%, Nickel 8.69%, Copper 0.66%, Sulphur 0.01% na Phosphorus 0.11.

Saturday, May 12, 2018

WAZIRI KIGWANGALLA AMTEUA MISS JOURNALISM TANZANIA 2018 KUWA BALOZI WA UTALII WA PORI LA AKIBA SELOUS

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na Miss Journalism Tanzania, 2018, Witness Teddy Kavumo (21) ambaye pia ni mshindi wa mwaka jana wa mataji manne ya Uanamitindo nchini Afrika ya Kusini, alipomtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuomba ufadhili wa kushiriki mashindano ya Dunia ya Miss Journalism yatakayofanyika Jijini Arusha mwezi Oktoba mwaka huu. Aidha, amemteua mwanamitindo huyo kuwa balozi wa utalii wa Pori la Akiba Selous. 

Na Hamza Temba-WMU-Dodoma
.............................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amemteua mshindi wa taji la Miss Journalism Tanzania, 2018, Witness Teddy Kavumo (21) kuwa balozi wa utalii wa Pori la Akiba Selous.

Amefanya uteuzi huo mwishoni mwa wiki Jijini Dodoma baada ya mazungumzo na mwanamitindo huyo aliyemtembelea ofisini kwake kwa ajili ya kuomba ufadhili wa kuandaa  mradi wa kijamii ambao ni sehemu ya shindano atakaloshiriki la taji la Dunia la Miss Journalism 2018 litakalofanyika Oktoba 27 Jijini Arusha.

Kufuatia uteuzi huo, Dk. Kigwangalla amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Devotha Mdachi kuandika barua ya uteuzi kwa balozi huyo mpya sambamba na kumkabidhi hati ya uteuzi ili pamoja na mambo mengine aweze kunadi vivutio vya utalii vya pori hilo.

Wakati huo huo, Dk. Kigwangalla amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, Dk. James Wakibara kuandaa safari maalum ya balozi huyo mteule aweze kutembelea Pori la Akiba Selous kwa ajili ya kuona na kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu hifadhi hiyo kwa ajili ya utangazaji.

Sambamba na pori hilo atatembelea pia mapori mengine ikiwemo BBK (Burigi, Biharamulo na Kimisi) mkoani Kagera na Mpanga Kipengele mkoani Njombe ambapo  atatumia fursa hiyo kufanya mahojiano na wasichana wa vijiji jirani na hifadhi hizo kwa ajili ya mradi wa kijamii wa kuwainua ikiwa ni sehemu yenye alama muhimu kwenye shindano hilo la Dunia la Miss Journalism 2018.

Awali akiwasilisha ombi lake kwa Waziri Kigwangalla la ufadhili wa safari yake ya ushiriki wa mashindano hayo, Witness pia aliomba kupewa fursa ya kuwa balozi wa Tanzania kwenye moja ya sekta ikiwemo Misitu, Nyuki au Utalii.

Mbali na kushikilia taji la Miss Journalism Tanzania 2018, Witness amesema amewahi kushinda mataji mengine manne makubwa ya kimataifa ya ulimbwende nchini Afrika ya Kusini anakosomea urubani kwa sasa.

Anasema, "Miongoni mwa mataji hayo ni Miss Garden Route 2017, ambalo ni taji la kitaifa la kuhamasisha na kukuza sekta ya Maliasili na Utalii nchini humo, licha ya kuwa ugenini nilitumia fursa hiyo kunadi vivutio vya utalii vya Tanzania. 

"Mashindano haya yalihusisha washiriki 600 na wote walikuwa na asili ya kizungu, mimi peke yangu nilikuwa na asili ya kiafrika na niliibuka mshindi". 

Aliyataja mataji mengine kuwa ni Miss Bees Cape Town 2017 kwa ajili kuhamasisha uhifadhi wa sekta ya nyuki na mataji mawili ya kimkoa ambayo ni Miss Asla Capetown 2017 na Miss Carnival Mosselbay 2017.

Mataji mengine ya kitaifa aliyowahi kushinda Witness hapa nchini ni pamoja na Miss Arusha Higher Learning 2014 na Miss Northern Zone 2014.

Mashindano hayo ya Dunia ya Miss Journalism 2018 yanahusisha pia uhamasishaji wa maendeleo ya utalii, utamaduni wa amani, uandishi wa habari na kupiga vita ugonjwa wa ukimwi na Malaria.

Pori la akiba Selous ndio hifadhi kubwa kuliko zote nchini ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba takriban 50,000 katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Lindi, Mtwara na Ruvuma. Mwaka 1982, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Uneso) lilitangaza eneo hilo kuwa moja ya eneo la Urithi wa Dunia na kuanza kuhifadhiwa.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akionyeshwa taji la urembo la "Miss Garden Route South Africa 2017" ambalo ni maalum kwa ajili ya kuhamasisha utalii nchini Afrika ya Kusini na Miss Journalism Tanzania 2018, Witness Teddy Kavumo (21) aliyeshinda taji hilo na mataji mengine matatu nchini humo mwaka jana, alipomtembelea ofisini kwake mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuomba ufadhili wa kushiriki kwenye mashindano ya Dunia ya Miss Journalism yatakayofanyika Jijini Arusha mwezi Oktoba mwaka huu. Aidha, amemteua mwanamitindo huyo kuwa balozi wa vivutio vya utalii vya Pori la Akiba Selous. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiwa kwenye picha ya pamoja na Miss Journalism Tanzania, 2018, Witness Teddy Kavumo (21) ambaye pia ni mshindi wa mwaka jana wa mataji manne ya Uanamitindo nchini Afrika ya Kusini, alipomtembelea ofisini kwake Jijini Dodoma mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuomba ufadhili wa kushiriki mashindano ya Dunia Miss Journalism yatakayofanyika Jinini Arusha mwezi Oktoba mwaka huu. Aidha, amemteua mwanamitindo huyo kuwa balozi wa vivutio vya utalii vya Pori la Akiba Selous.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akiagana na Miss Journalism Tanzania, 2018, Witness Teddy Kavumo (21) ambaye pia ni mshindi wa mwaka jana wa mataji manne ya Uanamitindo nchini Afrika ya Kusini, baada ya mazungumzo ofisini kwake Jijini Dodoma alipomtembelea mwishoni mwa wiki kwa ajili ya kuomba ufadhili wa kushiriki mashindano ya Dunia ya Miss Journalism yatakayofanyika Jinini Arusha mwezi Oktoba mwaka huu. Aidha, amemteua mwanamitindo huyo kuwa balozi wa wa utalii wa Pori la Akiba Selous.