slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Thursday, July 27, 2017

WAZIRI WA MALIASILI, PROF. JUMANNE ABDALLAH MAGHEMBE AFUNGUA MKUTANO WA MWAKA WA WAHARIRI NA WANAHABARI WAANDAMIZI ULIONDALIWA NA TANAPA JIJINI TANGA, AWATAKA KUTUMIA KALAMU ZAO KUELIMISHA JAMII KUHUSU UHIFADHI ENDELEVU

NA HAMZA TEMBA -WMU - TANGA
...................................................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe amevipongeza vyombo vya habari nchini kwa mchango wake katika vita dhidi ya ujangili huku akitoa rai kwa vyombo hivyo kuongeza bidii katika kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa uhifadhi endelevu wa maliasili za taifa kwa faida ya jamii iliyopo na vizazi vijavyo.
Prof. Maghembe ametoa pongezi na rai hiyo leo wakati akifungua mkutano wa sita wa mwaka wa wahariri na wanahabari waandamizi wa vyombo vyote vya habari nchini ulioandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) jijini Tanga huku kaulimbiu ya mkutano huo ikiwa UTALII WA TANZANIA YA UCHUMI WA VIWANDA.
"Ujangili bado upo, Majangili tumepambana nao kweli kweli, na ninyi wanahabari mmetusaidia sana katika kuhabarisha jamii juu ya matukio ya kukamatwa kwao na hukumu wanazozipata, jambo ambalo limesaidia kujenga uoga kwa watu kushiriki katika vitendo hivyo", alisema Maghembe.
Alisema hofu hiyo pamoja na jitihada za Serikali za kupambana na ujangili imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza matukio ya ujangili nchini hasa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ambapo mizoga ya tembo inayotokana na ujangili imepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha ni miaka iliyopita.
Akizungumzia changamoto ya mifugo kwenye maeneo ya hifadhi nchini amesema sheria za uhifadhi zinakataza watu kuingiza mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kisheria, hivyo ni wajibu kwa wanahabari kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa kutii sheria hizo.  "Ni vema wanahabari wakatumia kalamu zao vizuri kuelimisha jamii juu ya athari za muingiliano wa binadamu, mifugo na wanyamapori".
Alisema wanyamapori wanabeba virusi vya magonjwa mbalimbali ikiwemo homa ya bonde la ufa, ndigana, kifua kikuu, homa za vipindi (brucolosis) na kimeta, Magonjwa ambayo yanaweza pia kuambukiza mifugo na binaadamu wanaoishi karibu na wanyamapori. Alisema kuwa endapo muingiliano huo utaendelea kuwepo kwa muda mrefu unaweza kusababisha mlipuko mkubwa wa magonjwa hayo kwa binaadamu na mifugo hivyo kusababisha vifo vingi kwa wakati mmoja.
Prof. Maghembe alisema kumekuwepo na kisingizio cha kumega maeneo ya hifadhi nchini kwa ajili ya matumizi ya kawaida kutokana na ongezeko la wananchi jambo ambalo sio sahihi na kwamba njia pekee na salama ni kubadili mfumo wa matumizi ya rasilimali zilizopo ikiwepo ya ardhi kwa kutumia sayansi na teknolojia na kuweka matumizi bora ya ardhi kwa kulenga matokeo chanya.
Akizungumzia sekta ya utalii, Prof. Maghembe alisema wanahabari wanapaswa kuwa sehemu ya kukuza uchumi wa nchi kwa kushiriki moja kwa moja katika utoaji wa taarifa sahihi kwa Watanzania na wageni kuhusu sekta hiyo bila ubaguzi wa aina yeyote.
"Tuipende nchi yetu, tuitangaze na kuilinda, na katika habari hizi za uchumi tuweke itikadi zetu pembeni tuandike habari za kujenga nchi yetu", alisema Prof. Maghembe.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa, Alan Kijazi amesema sekta ya utalii inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni. Alisema asilimia 80 ya wageni wanaokuja nchini wanatembelea hifadhi za Taifa hususan za ukanda wa Kaskazini jambo ambalo linaweka msukumo wa kuendeleza na kutangaza hifadhi za nyanda zingine ili kuongeza idadi ya watalii na pato la taifa.
Akizungumzia mchango wa TANAPA katika uchumi wa taifa, Kijazi alisema mchango huo umeongezeka ambapo katika mwaka 2015/2016 ilichangia Shilingi bilioni 27 katika mfuko mkuu wa Serikali na mwaka 2016/2017 ikachangia bilioni 34 sawa na ongezeko la bilioni saba.
Pamoja na mafanikio hayo alisema jukumu la kuendeleza uhifadhi nchini haliwezi kufanikiwa kwa jitihada za Serikali pekee bila kushirikisha wananchi kupitia vyombo vya habari, Hivyo akatoa rai kwa wanahabari kuiunga mkono Serikali katika kunadi sera za uhifdhi endelevu kwa maslahi ya taifa.
Waziri wa Utalii na Maliasili Prof.Jumanne Maghembe akizungumza jambo alipokuwa akifungua Mkutano wa Sita wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa Wahariri na Waandishi waandamizi ulioanza kufanyika leo kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa jijini Tanga, ,ambapo kauli mbiu ya mkutano huo ni 'Utalii na Tanzania ya Viwanda'.
 
Baadhi ya Wahariri na Wanahabari waandamizi wakifuatilia yaliyokuwa yakijiri kwenye mkutano wa Wahariri wa Vyombo vya Habari na Waandishi Waandamizi ulioanza kufanyika leo kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa jijini Tanga, ulioandaliwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA),ambapo kauli mbiu ya mkutano huo ni 'Utalii na Tanzania ya Viwanda'.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga,Mh Martin Shigella akiwakaribisha wageni mbalimbali waliofika kuhudhuria mkutano wa mwaka wa Wahariri na Wanahabari waandamizi,uliofanyika kwenye ukumbi uliopo kwenye ofisi zake.Mkutano huo umebeba kauli kuu ambayo ni 'Utalii na Tanzania ya Viwanda'.
Mkurugenzi Mkuu wa Shrika la Hifadhi za Taifa,(TANAPA),Allan Kijazi akimkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Utalii na Maliasili Prof.Jumanne Maghembe kufungua Mkutano wa Sita wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa Wahariri na Waandishi waandamizi ulioanza kufanyika leo kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa jijini Tanga,ambapo kauli mbiu ya mkutano huo ni 'Utalii na Tanzania ya Viwanda'.
Mkurugenzi Mkuu wa Shrika la Hifadhi za Taifa,(TANAPA),Allan Kijazi akimkaribisha mgeni rasmi Waziri wa Utalii na Maliasili Prof.Jumanne Maghembe kufungua Mkutano wa Sita wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa Wahariri na Waandishi waandamizi ulioanza kufanyika leo kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa jijini Tanga,ambapo kauli mbiu ya mkutano huo ni 'Utalii na Tanzania ya Viwanda'.
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Pascal Shelutete akiwakaribisha wageni waalikwa mbalimbali waliofika kwenye Mkutano wa Sita wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kwa Wahariri na Waandishi waandamizi ulioanza kufanyika leo kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa jijini Tanga, ,ambapo kauli mbiu ya mkutano huo ni 'Utalii na Tanzania ya Viwanda'.
Mhariri Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd.Absalom Kibanda akitoa salamu za shukurani kwa waandaji wa mkutano pia na kueleza changamoto kadhaa zinazopaswa kurekebishwa/kufanyiwa kazi na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
Baadhi ya Wahariri wakibadilishana mawazo kabla ya kuanza kwa mkutano huo.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe, viongozi wa Serikali, Wahariri na Waandishi Waandamizi walioshiriki mkutano huo.


 (PICHA NA MICHUZI JR BLOG)

No comments:

Post a Comment