slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Friday, August 4, 2017

MHANDISI MAKANI ASISITIZA UHIFADHI SHIRIKISHI WA MALIASILI ZA TAIFA

Niabu Waziri wa Malisili na Utalii,Mhandisi Ramo Makani akizungumza na wananchi katika kijiji cha Mshiri wilayani Moshi ,alipotembelea kijiji hicho kusikiliza Changamoto zinazo wakabili hususani katika eneo la Nusu Maili lililopo chini ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro.
Mkazi wa Kijiji cha Mshiri akiwaslisha hoja yake kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani.

NA HAMZA TEMBA -WMU
...............................................................................

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo makani amesema  jukumu la uhifadhi wa Maliasili za taifa sio la Serikali pekee kwakua Maliasili hizo ni urithi wa taifa na kila mwananchi anapaswa  kujua kuwa ana jukumu la kulinda urithi huo kutokana na umuhimu wake kwa taifa na jamii kwa ujumla.

Makani amesema hayo juzi wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mshiri, Jimbo la Vunjo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro katika ziara yake ya siku mbili mkoani humo kwa ajili kuona changamoto za uhifadhi na kutatua migogoro ya ardhi kwenye maeneo yaliyohifadhiwa.

Alisema askari pekee na mitutu ya bunduki haitoshi kulinda maliasili hizo kutokana na ukubwa wa maeneo yaliyopo ukilinganisha na rasilimali zilizopo. "Maliasili hizi zipo kwa faida ya kila mwananchi, tunawaomba muendelee kuiunga mkono Serikali katika kulinda Maliasili tulizonazo, tunahitaji kufanya uhifadhi shirikishi, utalii uimarike na nchi yetu ipate mapato zaidi tuweze kufikia uchumi wa kati", alisema Makani.

Akitaja miongoni mwa faida hizo, Makani alisema maliasili za misitu husaidia upatikanaji wa mvua, kuweka mazingira bora kwa ajili ya kilimo na upatikanaji wa hewa safi. Kwa upande wa faida za kiuchumi alisema sekta hiyo kupitia utalii inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa na asilimi 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni.

Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, Betrita Loibooki alisema hifadhi hiyo imejenga mahusiano mazuri na wananchi wa vijiji jirani na kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kukabiliana na ujangili ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita hakuna tukio lolote la ujangili wa tembo lililoripotiwa katika hifadhi hiyo.

Betrita alisema katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la uwekaji wa vigingi vya mipaka kwenye maeneo ya hifadhi ili kuepuka migogoro na wananchi alisema jumla vigingi 290 vimewekwa kwa ushirikiano na wananchi kuzunguka hifadhi hiyo kwa urefu kwa kilomita 123 sawa na asilimia 100 ya lengo lililokusudiwa.


Kwa upande wa Wananchi wa kijiji hicho cha Mshiri ambacho kinapakana na Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro waliiomba Serikali iwalegezee masharti waweze kuingia na waume zao pamoja na vijana wao wa kiume katika eneo la Nusu Maili lililopo ndani ya hifadhi hiyo waweze kusaidiana kazi ya kukata majani ya mifugo na kuokota kuni.

Akitoa ombi hilo mbele ya Mhandisi Makani, mkazi wa kijiji hicho, Theresia Mtui alisema wanawake wa vijiji jirani na hifadhi hiyo wanaruhusiwa kuingia ndani ya eneo hilo kwa ajili ya kukata majani ya mifugo na kuokota kuni kavu lakini wanaume hawaruhusiwi.

Alisema wapo tayari kuhifadhi na kulinda mlima huo “Tunaomba mturuhusu na mtupe angalao miaka miwili au mitatu ya majaribio muone tutakavyolinda msitu huu”, alisema Mtui.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho, Estomi Benjamin Moshi alisema “Ombi letu turuhusiwe kuingia na kukata majani tu katika eneo hili, tupo tayari kuilinda hifadhi hii kwa taratibu tutakazopewa”.

Akijibu ombi hilo Naibu Waziri Makani alisema, ombi hilo litaenda kufanyiwa kazi kwa ushirikiano kati Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wakuu wa Wilaya zinazozunguka eneo hilo la hifadhi ambazo ni Moshi, Rombo, Hai na Siha, Wizara ya Maliasili na Utalii na TANAPA ambapo wananchi watapewa mrejesho wa ombi lao hilo.

Sheria za uhifadhi zinakataza mtu yeyote kuingia na kulisha mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ikiwa ni pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu, kutokana na umuhimu wa eneo hilo kwa wananchi wanaolizunguka na katika jitihada za Serikali kujenga uhifadhi shirikishi, Mwaka 2014 Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kilimanjaro iliruhusu wanawake pekee kuingia ndani ya eneo hilo umbali wa mita 800 kutoka kwenye mpaka wa hifadhi hiyo kwa ajili ya kukata majani ya mifugo na kuokota kuni, wanaume walizuiliwa kutokana na kujihusisha na uharibifu wa eneo hilo. 

Nae mbunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia alisema ili uhifadhi uimarike ni lazima uwepo ushirikiano wenye tija kwa Serikali, Wananchi na Hifadhi huku akitoa rai ushirikiano huo uimarishwe kwa maslahi ya pande zote.

No comments:

Post a Comment