slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Tuesday, August 1, 2017

MHANDISI MAKANI ASISITIZA UTALII WA MISITU YA ASILI NCHINI KAMA CHANZO MUHIMU CHA KUONGEZA PATO LA TAIFA NA JAMII KWA UJUMLA


Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akijibu kero mbalimbali za uhifadhi kwa wananchi wa Kijiji cha Shume Nywelo, Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo jana. 

NA HAMZA TEMBA - WMU
.........................................................................................
Katika kuhakikisha sekta ya utalii nchini inaendelea kukua kwa kasi, Serikali imesema itaimarisha utalii wa Misitu ya Asili nchini iweze kutoa mchango mkubwa kwenye pato la taifa tofauti na ilivyo hivi sasa ambapo hutegemea zaidi utalii wa wanyamapori.

Hayo yamesemwa jana wilayani Lushoto na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku moja wilayani humo kwa ajili ya kutatua migogoro mbalimbali ya uhifadhi.

Alisema sekta ya utalii nchini imekuwa ikitegemea sana wanyamapori na kusahau vivutio vingine kama vile misitu ya asili ambayo ndani yake kuna mimea na viumbe hai mbalimbali adimu duniani na ambavyo hupatikana Tanzania pekee.

“Tumezoea zaidi utalii wa wanyamapori, utalii wa misitu unaweza kuzidi hata wa wanyamapori, kwenye misitu yetu ya asili tunajivunia mimea adimu ya asili na viumbe hai mbali mbali kama vile ndege, vyura, vipepeo, mijusi nakadhalika, tunachotakiwa kufanya ni kutunza misitu yote ya asili, tuiboreshe na kuitangaza ili kupata watalii wengi zaidi na pato la taifa liendelee kukua”, alisema Makani.

Kwa mujibu wa tovuti ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Tanzania ina jumla ya Hifadhi za Misitu ya Asili 100, idadi ambayo ni kubwa ukilinganisha na hifadhi za taifa ambazo zipo 16 pekee, idadi hiyo kubwa pamoja na upekee wake inatoa fursa pana ya kuendeleza sekta ya utalii nchini.

Akizungumzia mafanikio, Makani alisema sekta hiyo inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa na asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni. Alisema pamoja na faida hizo, sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya uharibifu wa misitu ya asili ambayo ni muhimu kutafutiwa suluhu ya kudumu ili kunusuru misitu hiyo.

“Ni lazima tutafute njia endelevu ya ulinzi wa misitu, hatuwezi kuwa na askari wa kutosha, walinzi na mitutu, njia sahihi ni ulinzi shirikishi, tuwaelimishe wananchi umuhimu wa misitu na tuwaeleze watanufaikaje, tofauti na zile faida za ujumla za upatikanaji wa mvua na hali nzuri ya hewa, hii itasaidia sana kuwaleta karibu kwenye uhifadhi wa pamoja”, alisema Makani.

Akizungumza na wananchi wa kijiji Nywelo wilayani humo kuhusu mgogoro wa mpaka baina ya kijiji hicho na shamba la miti Shume, Makani alisema tatizo lililopo ni uelewa tofauti kuhusu mpaka huo baina ya pande hizo mbili,  hivyo akuagiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kutuma wataalamu wa upimaji waliopima eneo hilo awali waje wafanye uhakiki wa mpaka huo kwa kushirikisha uongozi wa wilaya, halmashauri na kijiji hicho ili kuondoa tofauti hizo na kumaliza mgogoro huo ndani ya wiki mbili zijazo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Januari Lugangika alisema wilaya yake inakabiliwa na changamoto mbalimbali za uharibifu wa mazingira ikiwemo ukataji wa miti ya asili, uchimbaji wa madini kwenye maeneo ya hifadhi, uchomaji moto misitu na uhaba wa watumishi.

Katika ziara yake hiyo wilayani Lushoto, Naibu Waziri Makani alitembelea Hifadhi ya Mazingira Asilia Magamba na Shamba la Miti la Shume, alifanya pia vikao vinne vya ndani na mkutano mmoja wa hadhara ambapo alijibu kero mbalimbali za wananchi.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kushoto) akisikiliza moja ya kero kuhusu uhifadhi kutoka kwa Abunio Abraham Shangali (wa pili kulia) ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Shume Nywelo, Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo. 
 Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (wa pili kulia) akizungumza na viongozi wa kikundi cha uhifadhi na utalii cha Friends of Usambara kilichopo Lushoto Mkoani Tanga wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo jana.
Naibu Waziri wa Maliasili, Mhandisi Ramo Makani (kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Januari Sigareti Lugangika katika kijiji cha Shume Nywelo wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutatua migogoro ya hifadhi wilayani humo jana.
Muwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, Mwalimu Elias Mkwilima akijibu baadhi ya hoja katika mkutano huo uliofanyika katika kijiji cha Nywelo jana wilayani Lushoto Mkoa wa Tanga.

No comments:

Post a Comment