slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Friday, January 5, 2018

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, DK. HAMISI KIGWANGALLA ATOA MAAGIZO MAZITO KWA TFS

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (wa pilia kulia) akisalimiana na viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, muda mfupi baada ya kuwasili makao makuu ya mamlaka hiyo mkoani Morogoro jana.

...................................................
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla ameugiza uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kukabidhi eneo la Kilomita za mraba 25 kutoka kwenye Hifadhi ya Msitu wa Morogoro unaosimamiwa na wakala huyo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za Makao Makuu ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Ametoa agizo hilo jana akiwa kwenye ziara ya siku mbili mkoani Morogoro ambapo alimuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mej. Jen. Gaudence Milanzi kuzikutanisha taasisi hizo ndani ya siku saba zijazo ili kukamilisha mchakato wa kumega eneo hilo na kukabidhiwa kwa Mamlaka hiyo ili taratibu za ujenzi ziweze kuanza.

Aidha, ameuagiza uongozi huo wa TFS kuweka vigingi vya mpaka katika eneo la hifadhi hiyo ya msitu ndani ya siku 30 zijazo huku akitoa muda huo huo kwa wananchi wote waliovamia eneo hilo kuondoka mara moja kwa hiari yao wenyewe kabla ya kuondolewa kwa nguvu.

Katika hatua nyingine, Dk. Kigwangalla amemuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala hiyo, Prof. Dos Santos Silayo kukabidhi mbao zaidi ya 400 zilizokamatwa hivi karibuni mkoani Morogoro baada kuvunwa kinyume cha Sheria kwa uongozi wa Mkoa huo ili zisaidie kutengeneza madawati ya shule za msingi.

Pamoja na mbao hizo amemuagiza pia mtendaji huyo kukabidhi kwa uongozi wa mkoa huo magunia 350 ya mkaa yaliyokamatwa katika kituo cha Tazara yakiwa yanasafirishwa kinyume cha Sheria ili yasambazwe kwenye shule za Sekondari mkoani humo.

Dk. Kigwangalla alitoa maagizo hayo jana wakati akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Morogoro inayoongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Steven Kebwe, ambapo alimuomba kusimamia zoezi hilo la ugawaji kikamilifu ili walengwa waweze kufikiwa.

Katika ziara hiyo ametembelea pia bonde la Kilombero ambalo ni chanzo kikubwa cha maji yanayotengeneza Stieglers Gorge ambapo Serikali ya awamu ya nne itajenga mradi mkubwa wa kuzalisha umeme wa megawatts 2100.
 Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla (wa pilia kulia) akisalimiana na viongozi na watumishi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania TAWA, muda mfupi baada ya kuwasili makao makuu ya mamlaka hiyo mkoani Morogoro jana.
Dk. Kigwangalla akizungumza na watumishi wa TAWA wakati wa ziara hiyo.

No comments:

Post a Comment