slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Friday, January 12, 2018

LAZIMA TUTAFUTE NAMNA MPYA YA KUJITAMBULISHA NDANI YA NCHI NA NJE YA NCHI-DK. HAMISI KIGWANGALLA




Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Khamis Kigwangalla (wa pili kushoto) akifuatilia mkutano wa uzinduzi wa Kamati ya Kitaifa ya kuandaa Utambulisho wa Utalii wa Tanzania katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Jijini Dar es Salaam tarehe 11/01/2018, Kutoka kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Aloyce Nzuki, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Bibi. Devotha Mdachi na Mwenyekiti Mwenza wa kamati hiyo Richard Rugimbana.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Khamis Kigwangalla akisisistiza jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Kamati ya Kitaifa ya Kuandaa Utambulisho wa Utalii wa Tanzania katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Taifa cha Utalii Jijini Dar es Salaam. Kamati hiyo yenye wajumbe 21 imeundwa na Mhe. Waziri kwa lengo la kupitia na kubuni mkakati mbadala wa namna ya kutangaza utalii wa Tanzania ndani na nje ya nchi.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Utambulisho wa Utalii wa Tanzania Bibi. Devotha Mdachi akielezea jambo mbele ya wajumbe wa kamati hiyo (hawapo pichani) mara baada ya kuzinduliwa rasmi kwa Kamati hiyo leo Jijini Dar es Salaam. 
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Khamis Kigwangalla (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Utambulisho wa Utalii wa Tanzania lmara baada ya uzinduzi wa kamati hiyo leo Jijini Dar es Salaam. Kamati hiyo yenye wajumbe 21 imeundwa na Mhe. Waziri kwa lengo la kupitia na kubuni mkakati mbadala wa namna ya kutangaza utalii wa Tanzania ndani na nje ya nchi.
BR3
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Utambulisho wa Utalii wa Tanzania wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Khamis Kigwangalla.

Na Mwandishi Wetu
...................................................
WAZIRI wa Maliasili na Utalii Dkt.Hamis Kigwangala amesema ipo haja ya kuwa na kauli mbiu ambayo itatumika kutangaza vivutio vyote vya utalii wa Tanzania katika mataifa mbalimbali duniani.

Amesema Tanzania imejaaliwa kuwa na maeneo mengi ya utalii lakini hayajafahamika kutokana na nguvu ndogo ya kuyatangaza kwake, hivyo kusababisha watalii wengi kufanya utalii katika maeneo machache ya utalii ukiwamo Mlima Kilimanjaro.

Dk.Kigwangala ametoa kauli hiyo jijini  Dar es Salaam jana wakati anazindua Kamati ya Kuandaa Utambulisho wa Utalii Tanzania na kusema kuwa kuna vivutio vingi ambavyo sasa ipo haja kubwa ya kuendelea kuvitangaza kwa nguvu zote.

Amesema wajumbe wa kamati watakuwa na jukumu la kuweka mikakati sahihi ya kuhakikisha utalii wa Tanzania unaendelea kutangazwa kwa lengo la kuongeza watalii wa ndani na nje ya nchi.

“Tunayo maeneo mengi ya utalii lakini yanayofahamika ni machache, kuna watalii wanakuja kwa ajili ya kwenda Mlima Klimanjaro na wengine Mbuga ya Serengeti wakati yapo maeneo mengi ya utalii. Lazima tutafute namna mpya ya kujitambulisha nadni ya nchi na nje ya nchi, tutangaze utalii wetu na hii kamati itatusaidia kutuongoza,”amesema Dk.Kigwangala.

Amewataka wajumbe wa kamati hiyo kutafuta kauli mbiu ambayo itautangaza utalii wa Tanzania katika nchi mbalimbali duniani.

“Iwe kauli mbiu ambayo itatutofautisha Tanzania na nchi nyingine kwenye mambo ya utalii na lazima tuwe na kauli mbiu ya kipekee katika kuutangaza utalii wetu na vivutio vyake vyote”amesema Dk.Kigwangala.

Amefafanua kuna Hifadhi za Taifa 16 lakini zinazotambulika ni chache tu, hivyo juhudi zinahitaji zaidi kutangaza vivuto vya utalii vilivyopo.

Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Kitaifa ya Utambulisho wa Utalii Tanzania Richard Lugimbana amemhakikishia Dk.Kigwangala kuwa wanatambua jukumu ambalo wamepewa na hivyo ni wajibu wao kuweka mikakati ambayo itasaidia kuutambulisha utalii wetu. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Devotha Mdachi amefafanua kamati hiyo ina jumla ya wajumbe 21 ambao wengi wao ni  watalaamu wa masoko.

Ameongeza utambulisho mpya kwa ajili ya kutangaza utalii wa Tanzania utaifanya nchi kuwa katika ramani nzuri ya kutambulika kwa vivutio vyake vya utalii.

No comments:

Post a Comment