slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Monday, April 16, 2018

MAAFISA WANYAMAPORI WATAKIWA KUTOA ELIMU KWA WANANCHI WANAOZUNGUKA MAENEO YA HIFADHI - NAIBU WAZIRI HASUNGA

 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Japhet Ngailonga Hasunga (wa pili kulia) akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi – Usimamizi wa Rasilimali za Wanyamapori wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Bw. David Kanyata alipokuwa akitoa maelekezo kwa Maafisa Hifadhi wa wanyamapori wa pori la la akiba la Mkungunero alipofanya ziara katika pori hilo jana Wilayani Kondoa.
 Maafisa hifadhi wa wanyamapori wa pori la akiba la Mkungunero wakimsikiliza Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Japhet Ngailonga Hasunga (hayupo pichani) wakati akitoa maelekezo ya namna bora ya usimamizi wa hifadhi za wanyamapori alipofanya ziara katika pori hilo jana Wilayani Kondoa.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Japhet Ngailonga Hasunga (wa pili kulia) akimsikiliza Kaimu Mkurugenzi – Usimamizi wa Rasilimali za Wanyamapori wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Bw. David Kanyata alipokuwa akimfafanulia jambo wakati wa kikao na  Maafisa Hifadhi wa wanyamapori wa pori la akiba la Mkungunero alipofanya ziara ya kutatua migogoro kati ya wafugaji na mamlaka ya hifadhi ya pori hilo jana Wilayani Kondoa. Wakwanza kulia kwake ni Meneja wa pori la akiba la Mkungunero Bw. Emmanuel M. Birasso na Meneja wa pori la akiba la Swaga Swaga Bw. Alfred Choya.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Japhet Ngailonga Hasunga (kushoto) akitoa maelekezo kwa  Kaimu Mkurugenzi  – Usimamizi wa Rasilimali za Wanyamapori wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Bw. David Kanyata wakati wa kikao na  Maafisa Hifadhi wa wanyamapori wa pori la akiba la Mkungunero alipofanya ziara ya kutatua migogoro kati ya wafugaji na mamlaka ya hifadhi ya pori hilo jana Wilayani Kondoa.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Japhet Ngailonga Hasunga (katikati) akitizama sehemu ya ng’ombe waliokamatwa na Maafisa wa wanyamapori wa pori la akiba la Mkungunero kwa kuingia katika hifadhi hiyo wakati  alipofanya ziara ya kutatua migogoro kati ya wafugaji na mamlaka ya hifadhi ya pori la Mkungunero jana Wilayani Kondoa, ambapo zaidi ya ng’ombe 250 wanashikiliwa. Kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi – Usimamiziwa Rasilimali za Wanyamapori wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Bw. David Kanyata na kulia kwake ni Kaimu Kamanda wa Polisi Wilaya ya Kondoa Bw. Juma Solomon Nyamwakirya.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Japhet Ngailonga Hasunga (katikati) akimsikiliza Diwani wa Kata ya Bumbuta Bw. Bashiru Mtoro (kulia) alipofanya ziara katika hifadhi ya pori la Mkungunero lililoko Wilayani Kondoa jana. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Bi. Sezaria Makota.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Japhet Ngailonga Hasunga (kulia) akimsikiliza Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kondoa Bi. Hija Suru (kushoto) alipofanya ziara katika hifadhi ya pori la Mkungunero lililoko Wilayani Kondoa jana. Kulia kwake  ni Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Bi. Sezaria Makota.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Japhet Ngailonga Hasunga (kulia) akimsikiliza Meneja wa pori la akiba la Mkungunero Bw. Emmanuel M. Birasso (kushoto) alipofanya ziara katika hifadhi ya pori la Mkungunero lililoko Wilayani Kondoa jana.
 Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Japhet Ngailonga Hasunga (kushoto) akimsikiliza Bw. Yohana Bilo ambaye ng’ombe wake wanashikiliwa na Maafisa Hifadhi wa pori la Mkungunero kwa kuingia katika pori hilo alipofanya ziara ya kutatua migogoro kati ya wafugaji na hifadhi ya pori hilo jana Wilayani Kondoa.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe.Japhet Ngailonga Hasunga (kushoto) akitoa maelekezo kwa wafugaji wa vijiji vinavyozunguka pori la akiba la Mkungunero alipofanya ziara ya kutatua migogoro kati ya wafugaji na hifadhi ya pori hilo jana Wilayani Kondoa.

Na Mwandishi Maalum-Kondoa, Dodoma
......................................................
Serikali imewataka Maafisa Wanyamapori nchini kujikita zaidi katika utoaji wa elimu kwa wananchi hususani wakulima na wafugaji wanaozunguka maeneo mbalimbali ya hifadhi nchini ili kuepusha migogoro kati ya wananchi na mamlaka za hifadhi zinazosimamia maeneo hayo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Japhet Hasunga alipotembelea Pori la Akiba la Mkungunero katika wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma kwa ajili ya kutatua mgogoro baina ya wafugaji wa vijiji vinavyozunguka pori hilo na uongozi wa pori hilo, ambapo zaidi ya ngombe mia mbili hamsini wanashikiliwa kwa uvamizi.

“Wekezeni nguvu kubwa katika kutoa elimu kwa wananchi wanaozunguka pori hili ili wafahamu umuhimu na manufaa ya kutunza hifadhi badala ya kusubiri ng’ombe waingie kwenye hifadhi ili muwakamate, kazi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori siyo kuwafilisi wananchi” amesema Naibu Waziri Hasunga

Ameeleza kuwa jukumu kubwa la maafisa hifadhi ni kuwaelimisha wananchi ili waweze kuzijua taratibu na sheria zinazosimamia hifadhi za wanyama pori hapa nchini jambo litakalo punguza kwa kiasi kikubwa migogoro.

Aidha amewataka wafanyakazi wa Pori la Akiba la Mkungunero kufanya kazi kwa bidii, ubunifu, kuzingatia maadili ya utumishi na kujiepusha na vitendo vya rushwa na unyanyasaji wa wananchi  kwani vitendo hivyo vinaichafua taswira ya Mamlaka  hiyo na kujenga sifa mbaya kwa askari wake.

“Serikali haitosita kumchukila hatua kali za kinidhamu Afisa yoyote atakaye jihusisha na vitendo vya rushwa na unyanyasaji, hivyo hakikisheni mnafanya kazi kwa weledi mkizingatia Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo iliyopo ili kuongeza ufanisi wa Mamlaka hii” aliongeza Hasunga.

Hasunga aliwaeleza wananchi ambao mifugo yao imekamatwa ndani ya pori hilo kukutana mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. Alisema sheria za uhifadhi haziruhusu kuingiza na kulisha mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Bi. Sezaria Makota ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kusimamia kwa karibu Mamlaka ya Usimamizi wa Pori la akiba la Mkungunero.

“Ninapenda kuishukuru Wizara kwa juhudi zake za dhati za kufuatilia na kusimamia kwa karibu shughuli za pori hili, tunaomba muendelee na juhudi hizi za kutoa elimu kwa maafisa hifadhi wa wanyamapori na kutatua migogoro ya pori hili”  alisisitiza Bi. Sezaria

Akitoa maelekezo kwa maafisa hifadhi wa pori la akiba la Mkungunero, Kaimu Mkurugenzi – Usimamizi wa Rasilimali za Wanyamapori wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Bw. David Kanyata amesema wamepokea maelekezo yote ya Naibu Waziri na watahakikisha wanayafanyia kazi kwa wakati muafaka.

“Tunaahidi kuyatekeleza kwa haraka maagizo yote ya Mhe. Naibu Waziri ili kwenda na kasi ya awamu ya tano” alifafanua Bw. Kanyata.

Meneja wa pori la akiba la Mkungunero Bw. Emmanuel M. Birasso ameeleza kuwa pori hilo lina faida kubwa kiuchumi na kijeolojia ikiwa ni pamoja na kuwa sehemu muhimu ya mazalia ya wanyamapori ambao wako hatarini kutoweka kama tembo, chui na duma.

Aliongeza kuwa, pamoja na umuhimu wa pori hilo bado kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili mamlaka ya pori hilo kama ujangili, uvamizi wa hifadhi kwa ajili ya kilimo, ufugaji na uchimbaji madini na  migogoro ya mipaka kati ya hifadhi na vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.

“Kumekuwa na changamoto kubwa ya uvamizi wa hifadhi kwa ajili ya shughuli za ufugaji ambapo mifugo 1320 na watuhumiwa 12 wamekamatwa hadi sasa  kwa makosa ya uvamizi” aliongeza Bw. Birasso.

Pori la akiba la Mkungunero lililopo Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, linazungukwa na vijiji vipatavyo 11 na lina ukubwa wa kilomita za mraba 743.95.

No comments:

Post a Comment