slider gif

slider gif

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

kilimanjaro CAN ONLY B CLIMBED FROM TZ

Friday, May 11, 2018

DK. KIGWANGALLA AFUNGUA WARSHA YA KITAIFA YA MAPITIO YA RASIMU YA SERA YA TAIFA YA UTALII YA MWAKA 2018 JIJINI DODOMA

Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla akifungua Warsha ya Kitaifa ya Mapitio ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018 Jijini Dodoma leo.
............................................

WAZIRI wa Maliasili na Utalii,Dk.Hamisi Kigwangalla amesema  Serikali itaendelea kutekeleza sera ya Taifa ya Utalii  kwa ushirikiano na wadau katika usimamizi, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za maliasili na utalii nchini.

Dk. Kigwangalla ametoa kauli hiyo Jijini Dodoma leo wakati akifungua warsha ya kitaifa ya mapitio ya rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018.

Amesema mafanikio ya sekta ya utalii yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uwepo wa Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 na juhudi za Serikali katika kutekeleza sera hiyo kwa ushirikiano na Wadau katika usimamizi, uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za utalii, utangazaji katika masoko mbalimbali ya utalii duniani na mazingira bora ya uwekezaji.

“Wote tunaelewa ya kuwa Utalii ni moja ya sekta zinazokua kwa kasi na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa nchi na kupunguza umasikini wa kipato”.

Amesema ukuaji wa sekta hiyo, umedhihirika pale ambapo katika miaka ya hivi karibuni mapato yatokanayo na utalii yaliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.7 mwaka 2012 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 2.2 mwaka 2017.

Amesema ongezeko la mapato hayo ni kutokana na ongezeko la idadi ya watalii kutoka 1,077,058 mwaka 2012 hadi kufikia watalii 1,327,143 mwaka 2017.

Waziri Kigwangalla amesema sekta ya utalii inachangia takriban asilimia 25 ya mapato yote ya fedha za kigeni (foreign exchange earnings).

Akizungumzia mambo yaliyowekewa mkazo katika rasimu hiyo amesema ni pamoja na Serikali kuendelea kushirikiana na wadau wote wa utalii katika kuhifadhi rasilimali za utalii.

“Kuendeleza rasilimali watu, kuimairisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, kuimarisha mnyororo wa thamani katika mazao ya utalii, kuongeza wigo wa mzao ya utalii kama vile kuendeleza utalii wa fukwe na utalii wa mikutano, kuweka mkazo katika kutangaza Tanzania kama kituo bora cha utalii kimataifa.

“Napenda kusisitiza kuwa, Sera hii itakuwa na nyenzo nyingine muhimu za kuitekeleza ambazo ni Mkakati wa utekelezaji wa Sera na Progamu ya Maendeleo ya Utalii nchini.

“Tayari Wizara imeanza maandalizi ya awali ya kukamilisha nyenzo hizo na mtashirikishwa kikamilifu katika kuziandaa na utekelezaji wake,”amesema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi amesema sera ya Taifa ya Utalii iliyopo hivi sasa ilifanyiwa mapitio kwa mara ya mwisho mwaka 1999 ambapo ni takribani miaka 18 iliyopita.

Amesema kwa kutambua hilo, Wizara iliona kuna umuhimu mkubwa kupitia upya Sera hiyo ili kuhakikisha ukuaji wa Sekta ya Utalii nchini unaenda sambamba na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani ikiwamo mabadiliko ya teknolojia, kijamii, kiuchumi, kisiasa na kimazingira.

Alisema kwa kuzingatia kuwa msingi mkuu wa kuandaa Sera yeyote ni kuwashirikisha wadau ambao ndio watekelezaji wa Sera hiyo, mapitio ya Sera hii, yameshirikisha wadau wote muhimu tangu hatua za awali.

“Kazi hii ilipangwa kufanyika kwa awamu tano (5) ambazo ni kukusanya maoni ya wadau katika kanda saba za Tanzania Bara na Zanzibar, uchambuzi wa maoni na kuandaa rasimu ya Sera, kuwasilisha rasimu ya Sera kwenye warsha ya kitaifa ambayo inafanyika leo na hatimaye kuandaa rasimu ya mwisho ya Sera na Mkakati wa Utekelezaji,” alisema.

Warsha hiyo imejumuisha wadau mbalimbali wa sekta ya umma na binafsi wanaohusika maendeleo ya sekta ya utalii nchini.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla akifungua Warsha ya Kitaifa ya Mapitio ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018 Jijini Dodoma leo.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akizungumza katika warsha hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi akizungumza katika warsha hiyo.
Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii Deogracious Mdam akizungumza katika warsha hiyo.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa ESRF, Deodatus Sagamiko akizumza katika warsha hiyo. ESRF ni moja ya wadau wakuu waliofadhili zoezi hilo la kuhuisha sera ya taifa ya utalii.
 Baadhi ya wadau katika wa warsha hiyo.
 Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo.
 Meza kuu.
 Wadau. 
  
 Picha ya pamoja.
 Picha ya pamoja.
 Picha ya pamoja.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudence Milanzi (katikati) akifurahia jambo na Naibu Katibu wa Wizara hiyo, Dk. Aloyce Nzuki (kulia) na Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Deogracious Mdam wakati Warsha ya Kitaifa ya Mapitio ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018 Jijini Dodoma leo.
 Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamisi Kigwangalla akiteta jambo na mdau wa utalii, Dk. Leaky Abdallah wakati wa Warsha ya Kitaifa ya Mapitio ya Rasimu ya Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 2018 Jijini Dodoma leo.
Baadhi ya wadau wa utalii kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii.

No comments:

Post a Comment